Amani katika Uwili wa Maisha.

Kufumba.Kufumbua.Kuwaza.Kuwazua.Kufunga.Kufungua.Kupata. Kupoteza.Kukwepa.Kupatikana.
Mbona yote yawe na mielekeo miwili?Mbona kuwe na baya na zuri?Kuna haja gani ya kufeli masomoni na ninaweza faulu?Hata aliyekuwa na hekima yote kuliko watu wote duniani alitambua yaya haya.Lakini kwake alitumia taswira tofauti.Solomoni anasema;kuna wakati wa kila jambo-wakati wa kulia na wakati wa kucheka,wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna,wakati wa kupata na kukosa na kwa hekima iliyomjaa anazidii kufafanua hili.Sitofaulu kuelekea katika kina cha hekima yake,waweza rejelea kitabu cha Mhubiri 3.

Kwa kuchagawa,nilifikia upeo wa tafakuri,maswali yakijibwaga akilini yakitishia kumiliki urazini.Upo uwezekano wa kuandamwa na mema bila kuyapata mabaya asilani?Kuna uwezekano wa bingwa kutoshindwa mpaka upeoni mwa maisha yake?Iwapo si mazuri basi;upo uwezekano wa mwanadamu kuandamwa na shida hadi mwisho,aingiapo kaburini?Mwanadamu anaweza kufuatwa na majanga au magonjwa ya kila aina mpaka tamati?Kama jawabu ni ndio,tutaelezaje msururu huo wa matukio?

Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo nina uhakika ipo sekunde kama si dakika ulijipata ukiwaza na kwa kutaka amani akilini,ukaamua kujitia hamnazo.Ipo hekima uliyo nayo iliyoelekea kukupa jawabu naamini.Vilevile upo ujuzi uliokutoa amani na kukufanya uishiwe na tamaa ya maisha.


Baada ya kutagusana na watu kadha wa kadha na kusikiza paukwa na pakawa zao,maswali haya yalielekea kujibiwa na vile vile kudhihiri wepesi wake.Naam,yupo mtu mmoja kama si wote ambaye hujiona kutumbukia kwenye matatizo-tatizo moja hadi lingine.Kwake maisha hayana maana.Wazazi waliaga dunia hata kabla awajue;mama aliaga akijifungua na baba kuuchukua uhai wake muda usio mrefu.Kana kwamba kuwa yatima haitoshi,hapati ulezi na usaidizi wa aina yoyote kutoka kwa nasaba yake,bali,baada ya kuzurura anapata makao mapipani.Mapipani anapata namna ya kuishi na kukidhi mahitaji yake,lakini katika harakati hizi,magonjwa na upweke yanamwandama.Labda kwako hii hadithi inaonekana kuwa ya kupangwa sana.

Barabara, hata kama kisa nilichokupa kinaonekana kuwa cha kupanga twaweza uchukua mfano wako.Ipo siku uliyoamka na kukata kauli kuwa maisha haya si ya haki?Matatizo yalijipa nafasi kwako bila wewe kuyakusudia.Na kwa sababu moja au nyingine,huwezi kuwa na maswali haya uwapo katika bahari ya furaha.Lazima uwe katika huzuni kiwango Fulani ndipo upate kujiuliza maswali haya.

Hapo awali nilisema nilielekea kupata jawabu.Nalo jawabu halikuwa mbali na hali zilizonifika.Hata kama hekima si mali ya kila mmoja,nilipata fursa ya kujipiga kidari-angalau methali “akili ni nywele ” ilipata fursa ya kutumika.Nilifahamu kuwa ipo sababu ya maisha kuchukua mikondo miwili.Mkondo wa kuelekeza maisha kuwa mazuri na mkondo wa maisha kuwa mabaya.Labda kwa muda mfupi niliringa kuwa niko katika ukoo wa Solomoni,kwa sababu si kawaida kupata  hekima kama hii.Haidhuru.

Nilipata kuelewa kutoka kwa mawazo pevu ya;nitahitaji maji nihisipo kiu au nitahitaji chakula nihisipo njaa.Ingawaje kuhisi njaa na kiu yanakaa masuala madogo, ulinganifu wake na matatizo hayo mengine maishani ni wa kipimo kilekile.Kwa sababu, nipatapo huzuni nitatia bidii ili kuipata furaha, lakini, nipatapo furaha siwezi tia bidii  nipate huzuni.

Samahani kwa kutumia vijielezi vingi lakini lilo la muhimu ni kuelewa ninaloelekea kukudhihirishia.Si kudhihirisha,labda ni kukufahamisha.Au kama si kukufahamisha ni kukukumbusha.Mwanzo,ipo haja ya mwalimu iwapo mtoto(mwanafunzi) ashautoa ujinga wake?Ipo haja ya rubani kama nishawasili nilipotaka kufika?Ipo haja ya barabara kama sihitaji kuipitia?Majibu ya maswali haya ni sawia na jibu la kuwepo na ‘uwili’(ubaya na uzuri) maishani.

Mara nyingi tujiambiapo kuwa twaandamwa na matatizo kuliko wengine huwa twajidanganya.Lakini,matatizo tunayopitia ndiyo hutoa fursa ya kuona jawabu kwa upana.Kwa leo sitaangazia njia za kuona jibu katika tatizo.Nitaangazia Mungu ajidhihirivyo.Utajuaje daktari asipokutibu au usiposikia sifa zake za utabibu?Ni katika hali ya kukosa chakula utatambua kuwa Mungu huwapa wana wake-hawaachi maskini waombe mkate,anawapa ndege wa angani chakula,sembuse binadamu.

Kwa maneno mengi au machache nisemalo ni,ndio tupate fursa ya kumuita Mungu mponyaji lazima pawe na ugonjwa wa kuponywa.Ndipo tumuite Mungu mwema lazima kuwe na hali anayobadili na kuifanya iwe nzuri.Ndipo Mungu aitwe msaidizi ni shauri amsaidie mtu katika hali ngumu.Ndipo aitwe Mungu mwenye wivu,lazime iwe dhahiri kuwa hataki kuugawa utukufu wake na yeyote Yule.Kwa hivyo,katika hali yoyote ile unayopitia jua ni ya kudhihirisha sifa moja au zaidi kukuhusu-kuwa wewe ni;mvumilivu,mpole,mwaminifu na kadhalika.Pia ni njia ya Mungu kujidhihiri kwa wingi wa sifa zake.Na kama kawaida,kabla sijakuaga,upo wimbo unaozungumzia sifa moja ya Mungu.Ni furaha yangu uusikizapo wimbo huu:Usiyeshindwa wa Bi.Sarah Kiarie.

Iwapo una nyimbo zinazozungumzia sifa nyingine zaidi waweza kuongeza orodha katika nafasi ya maoni. 

Nakushukuru kwa kujipa katika kusoma makala haya.

Comments

Popular Posts